Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama lajadili ujenzi wa amani baada ya migogoro

Baraza la Usalama lajadili ujenzi wa amani baada ya migogoro

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, leo limekutana kujadili suala la ujenzi wa amani pale migogoro inapomalizika. Taarifa kamili na Joshua Mmali.

(Taarifa ya Joshua)

Kikao cha leo cha Baraza la Usalama kimesimamiwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Chile, Heraldo Muñoz, na kuhutubiwa na naibu Katibu Mkuu, Jan Eliasson, ambaye amezungumza kuhusu ripoti ya Katibu Mkuu kuhusu ujenzi wa amani mara tu baada ya migogoro, akisisitiza umuhimu wa utashi wa wadau na mikakati yakinifu ya ujenzi wa amani.

“Ujenzi wa amani huwezeshwa zaidi pale wadau wa kisiasa, usalama na maendeleo wanapounga mkono mkakati wa pamoja na yakinifu wa kuimarisha amani.”

Bwana Eliasson amezungumzia mizozo ya hivi karibuni katika nchi za Jamhuri ya Afrika ya Kati na Sudan Kusini, na pia nchi za Afrika Magharibi zilizoathiriwa na tatizo la mlipuko wa Ebola, akisema nchi zote hizo zipo kwenye ajenda ya Kamisheni ya Umoja wa Mataifa ya ujenzi wa amani.

“Pamoja na kusababisha vifo, mlipuko wa Ebola pia umeathiri pakubwa ustawi wa kijamii na taasisi za kitaifa. Kama Kamisheni ya ujenzi wa amani ilivyosema katika mikutano yake ya awali kuhusu mlipuko huo, kuna haja ya usaidizi wa kina utakaowezesha uhimili wa taasisi za kitaifa na ukwamuaji wa haraka.”