Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maandalizi ya operesheni za kijeshi dhidi ya waasi wa FDLR yaanza

Maandalizi ya operesheni za kijeshi dhidi ya waasi wa FDLR yaanza

Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Stephane Dujarric, amesema maandalizi ya operesheni za kijeshi dhidi ya waasi wa FDLR waliopo mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC yameanza.

Hatua hii inakuja baada ya kumalizika kwa muda wa kujisalimisha kwa amani kwa kundi hilo tarehe 2, Januari.

Operesheni hizo za kijeshi zinajumuisha Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, MONUSCO, pamoja na jeshi la DRC.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini New York, Dujarric amesema operesheni za kijeshi zinapaswa kwenda sambamba na mkakati mzima wa kisiasa.

Aidha, msemaji huyo amesema, ikizingatiwa kwamba kundi hilo linaishi pamoja na jamii, itachukua muda kufikia malengo wanayoyataka. Halikadhalika, Dujarric amesema umoja wa mataifa umejifunza kutoka operesheni zingine za zamani ikiwemo ile iliyoshirikisha wanajeshi wengi kutoka Rwanda mwaka 2009.

Operesheni za kijeshi zinaweza kupunguza nguvu za FDLR lakini si kuwaondoa kwa hiyo suluhu la kijeshi linapaswa kwenda sambamba na mkakati unaojumuisha hatua zisizo za kijeshi.

FDLR, ambao wanajulikana kama Majeshi ya Ukombozi wa Rwanda, wameshukiwa kuwa miongoni mwa waliotekeleza mauaji ya kimbari  ya Rwanda mwaka 1994..