Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Israel iwe makini na maandamano kwenye maeneo ya Palestina: Zeid

UN Photo - Jean-Marc Ferre
Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu, Zeid Ra’ad Al Hussein. Picha:

Israel iwe makini na maandamano kwenye maeneo ya Palestina: Zeid

Kamishna Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Zeid Ra’ad Al Hussein ameisihi Israel ichukue hatua za dharura kusitisha majeruhi na vifo vinavyosababishwa na maandamano kwenye maeneo yanayokaliwa ya Palestina.

Amesema hatua hiyo iende sambamba na uchunguzi wa dhati wa matukio ya aina hiyo.

Kamishna Zeid amesema hayo kufuatia kifo cha Waziri wa Palestina Ziad Abu Ein kilichotokea wakati vikosi vya Israel vilipokabiliana na waandamanaji tarehe 10 mwezi huu.

Ziad alifariki dunia baada ya kushambuliwa na askari wa Israel wakati wa maandamano yaliyoambatana na upandaji wa miti ya mizeituni kwenye makazi ya walowezi wa Israeli yaliyojengwa kinyume cha sheria kwenye kijiji cha Turmus’aya kilichoko Ukingo wa Magharibi wa mto Jordan.

Kamishna Zeid pamoja na kusema kusema matukio yaliyotokea kabla ya kifo cha waziri huyo yanasikitisha na lazima yachunguzwe ametuma salamu za rambirambi kwa familia ya Ziad na kwa wananchi wa Palestina.

Amesema maandamano ya amani ni haki ya msingi na vikosi vya usalama ni lazima vijizuie na wazingatia viwango vya kimataifa pindi wanapokuwa wanayadhibiti.