Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ebola na taswira mkanganyiko, UNMEER sasa yajielekeza Mali

Harakati za kusafirisha wagonjwa wa Ebola huko Sierra Leone. (Picha:WHO/C. Black — in Sierra Leone.)

Ebola na taswira mkanganyiko, UNMEER sasa yajielekeza Mali

Taswira ya mwelekeo wa mlipuko wa Ebola ni mchanganyiko wa matumaini na hofu, amesema mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Ebola, David Nabarro wakati akihutubia Baraza la usalama la Umoja huo lililokutana kujadili amani na usalama barani Afrika , angazio likiwa ni Ebola.

Amewaambia wajumbe kuwa ushiriki wa jamii kwenye vita dhidi ya Ebola kumeleta matumaini mathalani Liberia ambako idadi ya maambukizi mapya inapungua ilihali kwingineko mathalani Mali, maeneo ya kaskazini mwa Guinea na Sierra Leone, visa vipya vinaibuka na kutia hofu hivyo ni vyema kuwa macho.

(Sauti ya Nabarro)

“Kwa hiyo ni lazima tuwe macho na tuendelee na juhudi hizi na vile vile kuwa tayari kubadili hatua zetu kulingana na hali itakavyokuwa. Tukizembea tu, idadi ya wagonjwa itaongezeka tena na itatugharimu. Mlipuko huu na tishio lake kwa ukanda husika na dunia nzima kwa ujumla hautakuwa umekwisha hadi pale mgonjwa wa mwisho atakapobainika, atengwe na apatiwe matibabu.”

Kwa mujibu wa Nabarro,  Umoja wa Mataifa bado una pengo la dola Milioni 600 katika ombi lake la dola Bilioni Moja na Nusu za kuwezesha kukabiliana na Ebola hadi mwakani.

Naye mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kushughulikia dharura ya Ebola Anthony Banbury amehutubia baraza kwa njia ya video kutoka Accra, Ghana akigusia kupatikana kwa visa vya Ebola Mali akisema wamepatiwa agizo na Katibu mkuu juu ya hatua za kuchukua.

(Sauti ya Banbury)

“Hii leo kufuatia mashauriano yake na Rais Keita wa Mali, Katibu Mkuu ametuagiza kufungua ofisi yetu mara moja huko Mali ili kusaidia harakati za Taifa za kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huo katika hali ilivvyo sasa kabla ya kusambaa zaidi nchini Mali.”

Bwana Banbury amesema mlipuko wa sasa wa Ebola hauajwahi kushuhudiwa na mbinu dhidi yake ni lazima ziwe za mchanganyiko.

Baraza la usalama lilishatangaza Ebola kuwa ni tishio la amani na usalama duniani.