Dalili za mkataba wa kusitisha mapigano Sudan Kusini zaanza kuonekana

Dalili za mkataba wa kusitisha mapigano Sudan Kusini zaanza kuonekana

Pande mbili zinazopigana huko Sudan Kusini zimeripotiwa kuwa katika hatua nzuri za kutia saini makubaliano ya kusitisha mapigano kufutia mazungumzo yanayoendelea huko Addis Ababa, Ethiopia.

Wawakilishi wa pande hizo Ateny Wek Ateny ambaye ni msemaji wa  Rais wa Sudan Kusini na Mabior Garang, msemaji wa upande wa upinzani walizungumza kwa njia ya simu na Radio Miraya kutoka Addis Ababa kunakofanyika mazungumzo hayo ambapo kwa mujibu wa Ateny makubaliano hayo yanaweza kutiwa saini Jumapili au Jumatatu.

Sauti ya Ateny..

“Kwa hiyo awamu ya kwanza ni kuhusu kumaliza chuki, suala ambalo ujumbe wetu umekuja hapa kwa mashauriano na watarejea hapa kutia saini iwapo upande mwingine nao utakuwa tayari kutia saini.”

Msemaji huyo wa serikali amekaririwa akieleza kuwa suala la wafungwa wa kisiasa litajadiliwa kando mara  baada ya kutiwa saini mkataba wa kusitisha mapigano.

Naye Mabior Garang kutoka upande wa upinzani akazungumzia msimamo wao..

(Sauti ya Mabior)

“Nafikiri kwa upande wetu tangu mwanzo tulitaka makubaliano ambayo tunaweza kukubaliana nayo na ambayo  hayatakwenda kinyume na misingi yetu. Kwa hiyo tunaridhika na makubaliano hayo na tuko tayari kutia saini.”