Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mali yaongeza jitihada za kupambana na Ebola

Ujumbe huu unamsihi msomaji anawe mikono kwa kutumia sabuni na maji mara kwa mara. (Picha:WHO)

Mali yaongeza jitihada za kupambana na Ebola

Rais wa Mali, Ibrahim Boubacar Keita, amewataka wananchi kuchukua tahadhari zote katika vita dhidi ya Ebola, akisema kuwa hawatafunga mpaka wa nchi hiyo, lakini akaongeza kwamba hakuna atakaye ruhusiwa kuingia nchini humo pasi na kunawa mikono au kupimwa joto. Taarifa kamili na Abdullahi Boru.

(Taarifa Abdullahi)

Kama hatua ya kudhibiti kuenea kwa ugojwa huo, serikali ya Mali imesema imewaweka watu karibu 600 wanaohofiwa kuambukizwa Ebola chini ya uangalizi wa kila siku.

Baada ya vifo vya Imam kutoka Guinea na muuguzi kutoka Mali, ambao walitibiwa katika kliniki ya Pasteur ilioko katika mji mkuu wa Bamako, rafiki aliyemtembelea Imam huyo pia amefariki dunia kwa kile kinachowezekana kuwa Ebola, huku daktari katika kliniki hiyo ambaye pia alianza kuumwa anafanyiwa matibabu.

Huku juhudi za kimataifa za kudhibiti kuenea kwa Ebola zikiendelea, Muungano wa Ulaya umetangaza dola milioni 15 za msaada kuzisaidia nchi za Mali, Senegal na Ivory Coast kujiandaa kwa ajili ya hatari ya Ebola kuzuka kupitia ugunduzi wa mapema na kuongeza ufahamu wa umma.