Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ajenda ya maendeleo baada ya 2015 izingatie nchi zinazoendelea zisizo na bandari- Kutesa

UN Photo/Devra Berkowitz
Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Sam Kutesa,(

Ajenda ya maendeleo baada ya 2015 izingatie nchi zinazoendelea zisizo na bandari- Kutesa

Rais wa Baraza Kuu, Sam Kutesa, amesema wakati ajenda ya maendeleo baada ya mwaka 2015 inapobuniwa, ni lazima kuhakikisha kuwa ni yenye kuleta mabadiliko, na inayonufaisha na kuboresha maisha ya kila mtu.

Bwana Kutesa amesema hayo leo mjini Vienna, Austria, wakati wa kufungua kongamano la siku tatu kuhusu nchi zinazoendelea zisizo na bandari.

Rais huyo wa Baraza Kuu amesema kuwa kuendeleza miundo mbinu, viwanda na usindikaji na kuongeza thamani bidhaa za kilimo ni masuala muhimu kwa maendeleo ya nchi zinazoendelea zisizo na bandari.

Katika muktadha huo, amesema itakuwa vyema jamii ya kimataifa ikizingatia zaidi mahitaji ya nchi zinazokabiliwa na changamoto za aina yake, kama vile zile zinazoendelea zisizo na bandari, na nchi za visiwa vidogo zinazoendelea.

“Mpango mpya wa kuchukua hatua utakaoafikiwa hapa Vienna, unapaswa kuzisaidia nchi zinazoendelea zisizo na bandari kuimarisha ushindani wao, kuchochea uwezo wa kuzalisha, kupanua aina za mauzo ya nje, kuimarisha uhimili wao kwa matatizo ya ndani na nje, na muhimu zaidi, kuhakikisha mustakhbali bora kwa raia wao milioni 450.”