Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ebola yatokomezwa rasmi Senegal, WHO yatoa pongezi

Picha@UN WHO

Ebola yatokomezwa rasmi Senegal, WHO yatoa pongezi

Shirika la afya duniani, WHO leo limetangaza rasmi kuwa Senegal imetokomeza ugonjwa wa Ebola na kuipongeza nchi hiyo kwa kufikia hatua hiyo.

Kisa cha Ebola huko Senegal kilithibitishwa tarehe 289 Agosti baada ya mtu mmoja aliyesafiri kwa barabara hadi mjini Dakar akitokea Guinea kuripotiwa kuwa na makaribiano na mgonjwa wa Ebola.

WHO imesema hatua zilizochukuliwa na Senegal kudhibiti ugonjwa huo ni mfano wa kuigwa juu ya kile kinachopaswa kufanywa pindi mgonjwa anaporipotiwa ili kuzuia kuenea kwake.

Hatua ambazo Senegal ilichukuwa pindi tu mgonjwa aliporipotiwa ilikuwa ni kubaini na kuwafuatilia watu 74 aliokuwa na karibu na kuwafanyia uchunguzi wa kina.

Halikadhalika Senegal iliimarisha ukaguzi na usimamizi kwenye vituo vyote vya mipakani pamoja na kampeni kwa umma dhidi ya Ebola.

Hata hivyo WHO imesema licha ya kwamba mlipuko umedhibitiwa, Senegal iko hatarini hivyo ni vyema kuendelea kuwa macho na kuzingatia miongozo ya WHO dhidi ya Ebola.