Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Siku ya wanawake wa vijijini, Ban ataka sauti na mahitaji yao visikilizwe

Wanawake wa kijijini licha ya mchango wao kwenye jamii bado mahitaji yao hayapatiwi kipaumbele. (Picha:UN /Albert González Farran)

Siku ya wanawake wa vijijini, Ban ataka sauti na mahitaji yao visikilizwe

Ikiwa leo ni siku ya kimataifa ya wanawake wa vijijini, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon amesema kundi hilo linaweza kuchagiza maendeleo ya dunia iwapo sauti na mahitaji yao yatazingatiwa. Taarifa kamili na Assumpta Massoi.

(Taarifa ya Assumpta)

Katika ujumbe wake Ban amesema licha ya kukosa elimu rasmi, wanawake hao akitolea mfano mama yake mzazi, wana busara, ustahimilivu na ufahamu wa hali ya juu ambao umesaidia familia nyingi kujikwamua.

Amesema wanawake hao mara nyingi wanakabiliwa na umaskini, majanga ya kiasili na vitisho vingine hivyo ni wadau wakubwa katika harakati za kufanikisha kampeni za kimataifa ikiwemo za mabadiliko ya tabianchi na malengo ya maendeleo ya milenia.

Ametaka siku ya kimataifa ya wanawake wa kijijini itumike kusikiliza sauti zao na kuchanua uwezo wao kwa kulinda haki zao za kibinadamu ili waweze kuchangia katika mustakhbali wa ustawi duniani.

Nalo Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na Masuala ya Wanawake, UN Women, limetaka kila mtu binafsi, serikali na Umoja wa Mataifa, kujitoa kwa dhati na kutambua michango na haki za wanawake wa vijijini, ikiwa ni pamoja na haki zao za umiliki wa ardhi na rasilimali.