Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tukisuasua, idadi ya wagonjwa wa Ebola kwa wiki itakuwa 10,000 ifikapo Disemba: UNMEER

Mkuu wa UNMEER Anthony Banbury. (Picha:UN/Eskinder Debebe)

Tukisuasua, idadi ya wagonjwa wa Ebola kwa wiki itakuwa 10,000 ifikapo Disemba: UNMEER

Idadi ya wagonjwa wapya wa Ebola inatarajiwa kuwa Elfu Kumi kwa wiki ifikapo Disemba Mosi mwaka huu iwapo hatua za haraka za kudhibiti hazitachukuliwa.

Hayo yamesemwa na Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na mkuu wa ofisi ya Umoja huo kuhusu dharura ya Ebola, UNMEER Anthony Banbury wakati akihutubia Baraza la Usalama kuhusu hali ya mlipuko.

Amesema kwa sasa Liberia, Sierra Leone na Guinea zinajitahidi kudhibiti, halikadhalika jamii ya kimataifa, lakini bado harakati hizo hazitatosheleza kudhibiti Ebola kwani kasi ya kuenea kwake ni kubwa kuliko kutokomeza.

(Sauti ya Banbury)

“Ni kwamba tudhibiti Ebola sasa au tukabiliane na hali ambayo kwa sasa hatuna mkakati. Ili kudhibiti tuangalie idadi tarajiwa ya maambukizi mapya Disemba Mosi. Mwenzangu kutoka WHO na UNMEER amesema ifikapo Disemba Mosi tunaweza kutarajia wagonjwa Elfu Kumi kwa wiki. Hii ina maana tunahitaji vitanda Elfu Saba kwa matibabu. Chini ya mpango wa sasa tunatarajia kuwa ifikapo Disemba Mosi tutakuwa na takribani vitanda Elfu Nne kwenye vituo vya kutiba Ebola.”

Mkuu huyo wa UNMEER amesema muda unasonga kasi, halikadhalika wigo wa maambukizi hivyo ni vyema kuchukua hatua zaidi kudhibiti ugonjwa huo.

(Sauti ya Banbury)

“Njia nzuri, njia bora zaidi kulinda watu walio katika nchi zisizo na maambukizi, ni kwa kusaidia wananchi wa Guinea, Liberia na Sierra Leone kutokomeza Ebola hapo ilipo sasa.”

Bwana Banbury amesema habari njema kuhusu Ebola ni kuwa njia za kutokomeza zinafahamika hivyo ni vyema jamii ya kimataifa kuunga mkono nchi zenye mlipuko ili kuutokomeza.

Naye Mkuu wa operesheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa Hervé Ladsous amezungumzia athari za Ebola nchiniLiberiaakikumbusha kwamba ujumbe wa Umoja wa Mataifa UNMIL umeanzishwa miaka 11 iliyopita na ulikuwa umefanikiwa kurejesha hali ya utulivu nchini humo, lakini sasa kuna wasiwasi…

(Sauti ya Ladsous)

 “ Kwanza  mivutano ya kisiasa na kijamii inaongezeka, mfumo wa afya unafilisika, uchumi unasimama, hayo yote yanasababisha kuzorotesha mwelekeo. Bahati mbaya, tunaona kwamba bado watu wanazidi kutoamini mamlaka za serikali”

Amesema tarehe 14 oktoba Liberia ilikuwa inatakiwa kuandaa uchaguzi wa maseneta, lakini hali haikuruhusu kutekeleza uchaguzi huo.

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa lilikutana kwa mashauriano kuhusu amani na usalama barani Afrika likijikita zaidi katika mlipuko wa Ebola na athari zake za kiusalama kwenye maeneo yenye mlipuko.