Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali mali bado ni tete, asema Ban: Rais Keita asema wamejizatiti kuleta amani.

Katibu Mkuu wa UM Ban Ki-Moon akiwa na Rais Ibrahim Boubacar Keita wa Mali kwenye Makao makuu ya UM. (Picha:UN/Eskinder Debebe)

Hali mali bado ni tete, asema Ban: Rais Keita asema wamejizatiti kuleta amani.

Mkutano wa ngazi ya juu wa kuonyesha mshikamano kwenye mchakato wa kisiasa unaondelea nchini Mali umefanyika Jumamosi kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa ambapo Katibu Mkuu Ban Ki-Moon amesema hali ya usalama nchini humo bado ni tete.

Amesema kaskazini mwa nchi hiyo mapigano yanayohusisha vikundi vilivyojihami yameendelea licha ya makubaliano lukuki yaliyotiwa saini akitaka vikundi hivyo kusitisha mapigano huku walinda amani wa Umoja wa Mataifa wakiendelea kushambuliwa bila kusahau raia waMali.

(Sauti ya Ban)

“Wanasaka kuvuruga mchakato wa kisiasa na kuzuia kurejea kwa hali ya kawaida ambayo wakazi wa Kaskazini mwa Mali wanahitaji. Nalaani vikali mashambulizi haya na natoa wito kwa pande zote nchini Mali kushirikiana kukabili mashambulizi haya na wahusika wafikishwe mbele ya sheria. Lakini mashambulizi haya hayatabadili azma ya Umoja wa Mataifa kusaidia harakati za wananchi wa Mali za kusaka amani.”

Rais Ibrahim Boubacar Keita, wa Mali akizungumza kwenye kikao hicho amesema tayari wameanza kutekeleza makubaliano yaOuagadougouya mwezi Juni mwaka 2013 ambayo pamoja na mambo mengine yanalenga kufikia makubaliano ya kina ya amani yatakayoumaliza mzozo nchini humo.

(Sauti ya Rais Keita)

“Tunaweza kumaliza mkwamo wa sasa iwapo kutakuwepo na nia njema na utashi wa kisiasa kutoka pande zote, na hii ndio maana nimewaalika raia wenzangu wa upande wa Kaskaizni kuweka kando tofauti zao ili tusonge mbele. Kwa upande wake Serikali ya Mali iko tayari kujadili njia zote ambazo zinaweza kutoa kanuni bora kuhusu taasisi za uongozi wa pamoja jumuishi za uongozi zitakazoweza kuendeleza maendeleo ya dhati kwa jami husika.”