Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Amani Jamhuri ya Afrika ya Kati yapatiwa msukumo kando ya mjadala mkuu wa UM

Mkuu wa operesheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa Hervé Ladsous. (Picha:UN/Eskinder Debebe)

Amani Jamhuri ya Afrika ya Kati yapatiwa msukumo kando ya mjadala mkuu wa UM

Kikao cha ngazi ya juu kuhusu Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR kimehitimishwa kwa kupitisha kwa kauli moja taarifa ya pamoja ambayo pamoja na mambo mengine inaunga mkono hatua zote za amani zilizofikiwa nchini humo ikiwemo kutiwa saini kwa makubaliano ya kusitisha mapigano huko Congo-Brazaville tarehe 23 Julai mwaka huu.

Kikao hicho kilichohudhuriwa na viongozi wa ngazi ya juu akiwemo Rais wa mpito wa CAR, Catherine Samba-Panza, nchi zinazochangia vikosi vya ulinzi wa amani na viongozi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa, kililenga utekelezaji wa makubaliano ya kumaliza chuki, mchakato wa kisiasa na mahitaji ya kibinadamu pamoja na shughuli za maendeleo baada ya mzozo.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kikao, Mkuu wa operesheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa Herve Ladsous alieleza kuwa taarifa hiyo ya pamoja inaashiria mshikamano wa jamii ya kimataifa katika mwelekeo wa amani huko CAR huku akitaja mambo yaliyopatiwa kipaumbele.

(sauti ya Ladsous)

Kukusanya makundi yaliyojihami, kuyapokonya silaha na hatimaye kuyajumuisha kwenye jamii, halafu mchakato wote wa kisiasa unaoendelea. Kwa hiyo nadhani washiriki wote leo  wamekubaliana na mwelekeo huo.”

Awali akifungua mkutano huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon aliwaeleza wajumbe kuwa ziara yake CAR mwezi Aprili mwaka huu ilimkutanisha na mambo machungu lakini kwa kuwa sasa hali ya amani inaimarika ni vyema kusaidia utekelezaji wa sitisho la chuki na mchakato wa kisiasa ambao ni jumuish na shirikishi.