Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Operesheni za ulinzi wa amani ziwe za kisasa zaidi: Rais Kagame

Walinda amani kutoka Rwanda walioko kwenye kikosi cha ulinzi wa amani cha Umoja wa Mataifa huko Sudan Kusini, UNMISS wakishiriki ujenzi wa shule moja kwenye mji wa Juba. (Picha:UN/JC McIlwaine)

Operesheni za ulinzi wa amani ziwe za kisasa zaidi: Rais Kagame

Suala la operesheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa limepatiwa kipaumbele kwenye kikao cha ngazi ya juu kwenye Makao Makuu ya Umoja huo mjini New York, kikao kilichoandaliwa na Marekani kikiangazia mchango unaoweza kutolewa na nchi wanachama kuimarisha operesheni hizo.

Akifungua mkutano huo Katibu Mkuu Ban Ki-Moon amesema operesheni hizo zimekuwa na umuhimu sana akitoa shukrani kwa nchi wanachama zinazojitolea wanajeshi, polisi na watendaji wa kiraia.

Hadi sasa kuna zaidi ya walinda amani 130,00 sehemu mbali mbali duniani, bara la Afrika likiwa na idadi kubwa ya operesheni  hizo.

Ban amesema operesheni hizo zinakumbwa na changamoto ya vifaa, usalama kuanzia Mali barani Afrika, milima ya Golani huko Mashariki ya Kati hadi Haiti huku mahitaji yakiongezeka kila uchao hivyo mipango zaidi inahitajika.

(Sauti ya Ban)

“Bila usaidizi mbali mbali na thabiti kutoka nchi wanachama, vikosi vya ulinzi wa amani haviwezi kupelekwa haraka, kufanya kazi zake salama na kwa mpango mahsusi au kulinda raia kwenye maeneo tofauti na hatarishi.”

Suala hilo la kuimarisha operesheni za ulinzi wa amani likapatiwa msisitizo na Rais Paul Kagame waRwanda.

(Sauti ya Rais Kagame)

“Mahitaji ya operesheni za ulinzi wa amani yanaongezeka kwa idadi, ubora na hata ugumu wake. Na hivyo ili kukidhi mahitaji hayo kwa ufanisi tunapaswa kufirikia jinsi ya kuboresha na kurekebisha mtazamo wetu kwa jambo hilo.”

Makamu Rais wa Marekani Joe Biden ambaye alikuwa mwenyekiti wa kikao hicho akatoa ombi kwa walinzi wa amani.

(Sauti Biden)

“Tunawasihi walinda amani kulinda raia huko Sudan Kusini na Jamhuri ya Afrika ya Kati, na huko Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, wajiepushe na ukatili wa kingono, na wasaidie mchakato wa amani huko Mali ilhali kunaibuka mashambulizi mabaya yanayofanywa na watu wenye misimamo mikali.”