Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNFPA yatoa mafunzo ya uzazi wa mpango huko Sudan Kusini

Picha: UNFPA

UNFPA yatoa mafunzo ya uzazi wa mpango huko Sudan Kusini

Shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu, UNFPA limeanza kutoa mafunzo ya uzazi wa mpango na hatua dhidi ya ukatili wa kijinsia na ubakaji kwa watoa huduma za kibinadamu huko Sudan Kusini. Taarifa zaidi na Amina Hassan.

(Taarifa ya Amina)

UNFPA imechukua hatua hiyo kutokana na ongezeko la idadi ya vifo vya wajawazito, matukio ya ubakaji na ukatili wa kijinsia ambavyo ni matokeo ya mzozo unaoendelea nchini humo hususan jimbo la Upper Nile.

Mafunzo hayo ya siku tatu yatawezesha watoa huduma hao hasa kwenye kituo cha hifadhi cha Malakal chenye wakimbizi ni 17,000, waweze kutoa huduma hiyo.

Millicent Obaso ni Mratibu wa afya ya uzazi na ukatili wa kijinsia huko Malakal.

(sauti ya Millicent)

"UNFPA inania  ya kuokoa maisha ya wanawake hawa kwa kutoa huduma ya aina hii katika vituo vya afya. Mafunzo haya ni muhimu sana kwa washiriki kwa wakati huu kwa sababu ingawa ukatili wa kijinsia ulikuwepo hapo zamani lakini kwa sasa umezidi mno kutokana na mgogoro ulioanza Desemba.  Mnafahamu ongezeko la ukatili wa kijinsia kwenye hali ya kivita halijaanzia Sudan Kusini. Kwanza njia bora ya kulishughulikia, ni kuwa na amani, watu wakiwa na amani, hawataki kuumiza mtu, angalau si kwa kiasi hiki."

UNFPA inasema kuibuka tena kwa mapigano huko jimbo la Upper Nile, ina maanisha kuwa idadi ya wakimbizi wa ndani inaweza kuongezeka, halikadhalika idadi ya matukio ya ubakaji, ukosefu wa huduma za afya ya uzazi na ukatili wa kijinsia na hivyo ni vyema kuchukua hatua za kulinda afya za wakimbizi hao.