Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ubia mpya wazinduliwa kuokoa misitu ya dunia

Upandaji miti unasaidia kufyonza hewa ya ukaa inayosababisha ongezeko la joto duniani. (Picha@Joshua Mmali)

Ubia mpya wazinduliwa kuokoa misitu ya dunia

Juhudi za kupambana na mabadiliko ya tabianchi na kuboresha maisha kwa kulinda misitu zimepewa msukumo mpya leo kufuatia kuzinduliwa kwa ubia mpya kati ya Shirika la Mpango wa Mazingira, UNEP na Muungano wa Kimataifa wa Kuhifadhi Maliasili, IUCN, wiki chache kabla ya kilele cha mkutano wa Katibu Mkuu kuhusu tabianchi mnamo Septemba 23.

Ushirikiano huo unalenga kurejesha misitu iliyoharibiwa kwa kuhakikisha kuna tena ekari milioni 150 za misitu ifikapo mwaka 2020.

Ushirikiano huo utaleta pamoja mikakati miwili muhimu ya kimataifa inayoendelea ya kuokoa ardhi iliyomomonyoka, ambayo ni Mpango wa pamoja wa Umoja wa Mataifa wa Kupunguza Uchafuzi utokanao na Uharibifu wa Misitu, UN-REDD na Ubia wa Kimataifa kuhusu Kuokoa kwa Ardhi ya Misitu.

Kurejesha ekari milioni 150 za misitu iliyoharibiwa, ambazo zinalinganishwa na eneo la jimbo la Alaska Marekani au nusu ya eneo la ardhi ya India, kunakadiriwa kuwa kutasaidia kuondoa tani bilioni moja ya gesi chafuzi ya kaboni kutoka angani kila mwaka, na hivyo kupunguza pengo la uchafuzi kwa asilimia 11-17.