Baraza la Usalama lataka kikundi cha Houthi huko Yemen kiache uhasama dhidi ya serikali

29 Agosti 2014

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepitisha taarifa ya Rais wa Baraza hilo kuhusu hali ya siasa na amani nchini Yemen ambapo pamoja na mambo mengine inataka kikundi cha Houthi kiondoe vikosi vyake eneo la Amran.

Taarifa ilipitishwa kwa kauli moja na wajumbe wote wa baraza hilo ambapo pia inataka kikundi hicho kiache vitendo vyake vya kihasama dhidi ya serikali ya Yemen kwenye jimbo la Al-Jawf.

Punde baada ya taarifa hiyo kupitishwa, Balozi Mark Lyall Grant wa Uingereza ambaye ni Rais wa Baraza hilo kwa mwezi wa Agosti akawaeleza waandishi wa habari kwa muhtasari kilichojiri.

(Sauti ya Balozi Grant)

"Wajumbe wote wa baraza la usalama walikuwa kitu kimoja, kama ambavyo wamekuwa siku zote kuhusu Yemen katika kipindi cha miaka mitatu cha mpito. Na wameridhia ujumbe thabiti uliopelekwa kwa pande za mzozo huo kupitia taarifa hiyo ya Rais wa Baraza. Halikadhalika wajumbe wametoa shukrani za dhati na kuunga mkono jitihada za Benomar nchini Yemen. Na baraza limesema liko tayari kuchukua hatua zaidi ikiwemo vikwazo iwapo hali italazimu kufanya hivyo.”

Naye mshauri maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Yemen Jamal Benomar ambaye pia alipatia muhtasari baraza la usalama juu ya hali ilivyo nchini Yemen, akaeleza alivyopokea kupitishwa kwa taarifa hiyo.

(Sauti ya Benomar)

 "Naunga mkono kupitishwa kwa kauli moja kwa taarifa ya Rais wa Baraza na wajumbe. Kwa mara nyingine baraza limezungumza kwa kauli moja na kuunga mkono mchakato wa kisiasa Yemen. Wamerejelea kumuunga mkono Rais Abed Rabbo Mansour Hadi katika jitihada zake za kushughulikia hofu ya pande zote kupitia mjadala wa kitaifa wa maridhiano,.”

 Wakati huo huo, Baraza la Usalama limepitisha azimio kuhusu ulinzi wa watoa huduma za kibinadamu kwa kuzingatia ongezeko la vitisho na mashambulizi dhidi ya wafanyakazi hao.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter