Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Usalama Bangui unatia moyo, lakini viungani bado: Gaye

Babacar Gaye, Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa UM huko CAR na Mkuu wa MINUSCA. (Picha:UN/JC McIlwaine)

Usalama Bangui unatia moyo, lakini viungani bado: Gaye

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo limepokea ripoti kuhusu hali ya usalama huko Jamhuri ya Afrika ya Katim, CAR wakati ambapo siku zinahesabika kabla kikosi cha kulinda amani cha umoja huo kuanza kazi yake nchini humo tarehe 15 mwezi ujao.

Ripoti iliwasilishwa na mwakillishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini humo Luteni Jenerali Babacar Gaye ambaye amesema hali ya usalama kwenye mji mkuu Bangui angalau inatia moyo, idadi ya wakimbizi wa ndani imepungua na hata wananchi wanaweza kuendelea na shughuli zao za kawaida.

Hata hivyo amesema viungani na miji ya jirani hali si shwari.

(Sauti ya Gaye)

"Mapigano huko Batangafo na Bria hivi karibuni ni ishara dhahiri kwamba hali ya usalama bado inayumbayumba na kwamba wananchi wanasalia hatarini katika maeneo mengi nchini.Watu 26 waliuawa wakiwemo walinda amani wawili wa MISCA kufuatia mashambuliano kati ya waasi wa anti balaka na Seleka huko Batangafo mnamo Julai 31 yakifuatiwa na mapigano ya kujibu shambulizi hilo".

Luteni Jenerali Gaye ambaye pia ni Mkuu wa ujumbe wa kuweka utulivu huko CAR, MINUSCA amesema maandalizi yanaendelea kwa ajili ya vikosi vya kulinda amani ikiwemo kufungua ofisi mashinani kwa kabla ya tarehe 15 mwezi ujao sababu..

(Sauti ya Gaye)

"Uwepo wa wanajeshi, polisi na watendaji wa kiraia wa MINUSCA nje ya Bangui utakuwa muhimu katika kuimarisha maisha ya wananchi na kuweka mazingira sahihi ili amani endelevu iweze kukita mizizi".

Ameliomba Baraza la Usalama kuongeza uungaji mkono wake harakati za kurejesha amani CAR kwani raia ndio wanaoumia wakishindwa kuendelea na maisha yao ya kila siku.