Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Viongozi wa Sudan Kusini bado waamini silaha ni suluhu ya mzozo wao

Viongozi wa Sudan Kusini bado waamini silaha ni suluhu ya mzozo wao

Baraza la Usalama leo limekutana kutathmini  hali iliyopo Sudan Kusini na mahitaji ya Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, UNMISS.

Naibu Mkuu wa masuala ya operesheni za ulinzi wa amani kwenye Umoja wa Mataifa Edmond Mulet  amelieleza baraza hilo kwamba mashambulizi yanaendelea, waasi wengine wakilenga raia kwa misingi ya kikabila. Amesema, mapigano yanakwamisha shughuli za UNMISS, hasa katika usafiri wake.

Halikadhalika amesema, UNMISS inakabiliana na changamoto nyingi kutokana na kuendelea kupokea zaidi ya wakimbizi 95,000 ndani ya kambi zake ambazo hazikujengwa awali kwa ajili hiyo. Matatizo hayo ni pamoja na ukosefu wa usalama, usafi, afya na ufadhili kwa ujumla, hapo akisema

“ Kiwango cha operesheni za kibinadamu Sudan Kusini kimefikia kiwango cha operesheni kubwa zaidi ya kibinadamu duniani. Hata hivyo, uwezo na ufadhili wa operesheni hiyo ya kibinadamu hautoshi kulingana na mahitaji yaliyozidi. Watu milioni 4 wanakabiliwa na ukosefu wa usalama wa chakula, wakati nchi iko hatarini ya kukumbwa na janga la njaa”

Ameongeza, watoto 50,000 wako hatarini kufariki dunia kwa sababu ya utapiamlo wa kupindukia, na tayari mlipuko wa kipindupindu umeshasababisha vifo 150.

Amesema, mazungumzo ya amani yamerejea tarehe 5 Agosti ili kuunda serikali mpya ya muungano, akitoa wito kwa viongozi wa Sudan Kusini wawajibike kwa ajili ya raia wao:

“ Miaka mitatu baada ya uhuru, Sudan Kusini inakaribia kuporomoka sababu ya hali ya kibinadamu na mzozo wa kisiasa. Mzozo huu umesababishwa na binadamu, na wale waliousababisha wamechelewa kuutatua. Pande zote mbili zinaendelea kuamini kwamba watapata mafanikio zaidi wakiendelea kupigana”