Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

GAZA: Baada ya mapigano kusitishwa, UNDP yawekea kipaumbele ukarabati na ajira

Helen Clark. Mkuu wa UNDP. Picha: UNDP

GAZA: Baada ya mapigano kusitishwa, UNDP yawekea kipaumbele ukarabati na ajira

Shirika la mpango wa maendeleo la Umoja wa Mataifa UNDP limekaribisha sitisho la mapigano huko Ukanda wa Gaza likisema kwamba sasa litajikita kusaidia wapalestina wapate mahitaji yao.

Mkuu wa UNDP, Helen Clark, amesema hatua hiyo ni muhimu kwani nyumba za watu takriban 65,000 zimebomolewa ama kuharibika kwa kiasi fulani, akiongeza kwamba hiyo itawarudisha nyuma maendeleo yao wakati tayari hali yao ilikuwa si nzuri hata kabla ya mapigano.

Amesema kipaumbele cha UNDPni kuondoa vifusi vilivyotokana na majengo yaliyobolewa kutokana na mashambulizi na kurejesha mifumo ya maji safi, kujenga nyumba upya na kuwapatia watu ajira.

Bi. Clark amesema wakazi wa Gaza wameteseka mno, na hivi ni muda wa mabadiliko ili kuleta maendeleo ambayo raia wanataka.

Amesema mabadiliko hayo yanawezekana alimradi kunakuwepo na amani na misaada ya kimataifa.

Mkuu huyo wa UNDP ameunga mkono kauli ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon ya kuzitaka pande zote kwenye mzozo wa Gaza zijitahidi kupatia suluhu misingi ya mzozo huo, akisisitiza umuhimu wa kuondoa kitengo cha kuzingirwa kwa ukanda wa Gaza, na kutoendelea na hali iliyopo hivi sasa.