Baraza la Usalama lasikitishwa na hali ya kibinadamu Gaza

31 Julai 2014

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limekutana kwa dharura leo tarehe 31 Julai, kufuatia kuzorota zaidi kwa hali ya kibinadamu kwenye Ukanda wa Gaza, na kuuawa kwa watu 19 kwenye shule moja ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Palestina, UNRWA.

Mkuu wa Ofisi ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu, OCHA, Valerie Amos, amelielezea baraza hilo kwamba mzizi mmoja wa mzozo unaoendelea ni hali ya kuzingirwa inayowazuia Wagaza kuendesha shughuli zao za kiuchumi ama kupata chakula, akisema tayari hata kabla ya mapigano, zaidi ya asilimia 80 ya wa gaza walikuwa wanategemea misaada ya chakula.

Amelaani mashambulizi dhidi ya majengo ya Umoja wa Mataifa.

“ Kulingana na sheria ya kimataifa, serikali ya Israel, Hamas, na makundi mengine ya kijeshi wanapaswa kutofautisha malengo ya kijeshi na majengo ya kiraia, askari na raia. Wanapaswa pia kujizuia kuwadhuru raia au mali zao, na kuwalinda na matokeo ya operesheni za kijeshi. Jinsi nilishaliambia baraza hili, hata vita vina sheria”

Kwa upande wake Pierre Krahenbuhl, mkuu wa UNRWA, ameeleza kwamba ametembelea hospitali moja ya Gaza akiumizwa sana na kuona hali ya mtoto mmoja wa miezi mitano ambaye alijeruhiwa vibaya kwenye mashambulizi ya jana.

“ Watoto wa kipalestina niliowaona leo si takwimu, ni binadamu, na chini ya kila kifo ama jeraha, kuna maisha na hatma ya kuheshimu”

Ameiomba serikali ya Israel itekeleze uchunguzi dhidi ya uhalifu huo wa kivita akirejelea wito wa Katibu Mkuu kwa uwajibikaji wa mashambulizi hayo.

Kutokana na mtazamo wa Marekani kuhusu swala la Palestina, Baraza la Usalama halitarajii kupitisha azimio juu ya mada hiyo.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud