Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kenya yatakiwa kuwapatia wananchi wake huduma ya maji safi

Picha: World Bank/Allison Kwesell

Kenya yatakiwa kuwapatia wananchi wake huduma ya maji safi

Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa juu ya haki ya maji safi ya kunywa Catarina de Albuquerque ameitaka Serikali ya Kenya kutekeleza kwa vitendo katiba inayotoa haki kwa kila mwananchi wa Kenya kuwa na fursa ya kupata maji safi na salama.

Mtaalamu huyo ametoa wito huo mwishoni mwa ziara yake ya siku saba na kuongeza kwamba ni wajibu wa serikali kutekeleza kwa vitendo katiba hiyo ili kuhakikisha mamilioni ya wananchi wa Kenya wanapata haki yao.Taarifa zaidi na Amina Hassan

Taarifa ya Amina

Mjumbe huyo amelitaka Bunge la nchi hiyo kupitisha sheria ya maji na wakati huo huo amesema serikali inapaswa kuandaa mkakati wa kitaifa kuhusu maji ambao utatekelezwa katika maeneo yote ya nchi.

Inaarifiwa kuwa asilimia 30 tu ya wananchi wote wa Kenya ndio wanayo fursa ya kufikiwa na mifumo ya kujisafi na maji salama.

Amesema kuwa akiwa nchini humo alitembelea eneo la Turkana na kubaini kuwa zaidi ya asilimia 80 ya wakazi wa eneo hilo wanajisaidia katika maeneo ya wazi.

Amesema kuwa kitendo hicho siyo tu kwamba kinawanyima fursa ya kufikiwa na huduma safi na salama lakini pia kinazua tishio kuhusu afya ya jamii na jambo kubwa zaidi ni kuhatarisha usalama wa wanawake na watoto wa kike ambao wanalazimika kwenda kwenye misitu nyakati za usiku.