Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukraine yaishutumu Urusi kwa kusaidia waasi nchini humo

UN Photo/Mark Garten)
Yuriy Sergeyev, Balozi wa Ukraine katika Umoja wa Mataifa. Picha@

Ukraine yaishutumu Urusi kwa kusaidia waasi nchini humo

Ukraine imeikabidhi Uholanzi jukumu la kufanya uchugunzi kuhusu ndege ya MH17, kwa sababu wahanga wengi walikuwa na uraia wa Uholanzi, kwa mujibu wa Yuriy Sergeyev, Balozi wake wa Kudumu katika Umoja wa Mataifa.

Akizungumza na waandishi wa habari, amesema Ukraine ina uhakika kwamba waasi wanaotawala eneo hilo ndio walioitungua ndege hiyo na wanaendelea kupiga makombora huko ili ushahidi wa uhalifu wao upotee.

Amesema pia tukio hilo ni uhalifu wa kivita, kwa misingi ya kulenga ndege ya raia wa kawaida, kutoheshimu maiti za wahanga na kujaribu kuondoa ushahidi.

Balozi ameishutumu Urusi kwa kuendelea kusaidia waasi hao wanaopigana kwenye maeneo hayo ya mashariki mwa Ukraine, akiongeza kuwa jeshi la Ukraine limethibitisha kwamba jeshi la Urusi lenyewe linarusha makombora kutoka Urusi kwenda Ukraine.