Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Siku 15 tangu mzozo wa Gaza kuanza, hakuna muda wa kupoteza: Ban

Siku 15 tangu mzozo wa Gaza kuanza, hakuna muda wa kupoteza: Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, ambaye yupo ziarani Mashariki ya Kati, amewahutubia waandishi wa habari muda mfupi baada ya kukutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry.

Alipoulizwa kuhusu ni kwa nini akakubali kutumia ndege iliyofadhiliwa na Qatar kwa usafiri wake, Ban amesema:

“Hii ni siku ya 15 tangu mzozo huu ulipoanza. Hatuna muda mwingi wa kusubiri na kupoteza. Nashukuru juhudi yakinifu za Waziri Kerry za mashauriano na viongozi wa kimataifa, jinsi mimi mwenyewe nimekuwa nikifanya. Pamoja, tunaleta pamoja nguvu na juhudi zetu kuhakikisha usitishaji mapigano haraka iwezekanavyo. Lakini bado kuna masuala kadhaa ya kushughulikia. Ndiyo maana nakutana na Waziri Kerry kwa mara ya pili. Lakini tutaendelea kulijadili suala hili. Nimezungumza na Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu na nawasiliana pia na wote wanaojali, na ambao wanaweza kuwa na ushawishi kidogo katika kusaidia juhudi zetu za pamoja, na vile vile kushirikiana ili kuumaliza mzozo huu haraka iwezekanavyo.”

Mapema Asubuhi, Ban alikutana na Rais wa Israel, Shimon Peres, na baadaye amesafiri kwenda Saudia Arabia, kutoka Amman, Jordan. Ban amekuwa katika ziara hiyo ya Mashariki ya Kati tangu mwishoni mwa wiki iliyopita, akilenga kupatia suluhu mzozo unaotokota Mashariki ya Kati, ambao sasa umeyakatili maisha ya raia wengi.

Taarifa kamili kwa kiingereza.