Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu unafanyika Gaza: Pillay

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu katika Umoja wa Mataifa, Navi Pillay(Picha ya UM)

Ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu unafanyika Gaza: Pillay

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu Navi Pillay, ameilaani Israel kwa kutofanya kila iwezalo kulinda maisha ya raia wa Gaza, akisema kuwa kuna uwezekano mkubwa kuwa sheria ya kimataifa ya kibinadamu imekiukwa katika njia inayoweza kuchukuliwa kuwa uhalifu wa kivita.

Akilihutubia Baraza la Haki za Binadamu mwanzoni mwa kikao maalum cha kujadili hali huko Gaza, Bi Pillay amesema zaidi ya asilimia 70 ya wale waliouawa Gaza tangu mwanzoni mwa operesheni za kijeshi za Israel hivi karibuni ni raia. Amesema kutokuwepo kutofautisha kati ya raia na wapiganaji kumesababisha vifo vya watoto wengi wa Palestina.

Kamishna Mkuu huyo amesema kuwa mashambulizi ya kiholela ya roketi zaidi ya 2,900 zilizovurumishwa Israel na Hamas na makundi mengine yaliyojihami, pia hayakubaliki, akizingatia kuwa raia wa Israel pia wana haki ya kuishi bila hofu.

Zaidi ya Wapalestina 600, wakiwemo watoto wapatao 147 na wanawake 74, wameuawa kufikia sasa, huku raia wawili wa Israel wakiuawa kwa roketi zilizovurumishwa kutoka Gaza.

"Kupuuza huku kwa sheria ya kibinadamu ya kimataifa na haki ya uhai ni dhahiri kwa wote katika mashambulizi ya Julai 16 yaliowalenga watoto saba waliokuwa wakicheza katika pwani ya Gaza. Watoto hao walikuwa ni raia na hawakuwa wakitenda vitendo vya ghasia. Ninaarudia wito wangu kwa pande husika katika mzozo, kwamba raia wasilengwe. Kuheshimu haki ya kuishi, wakiwemo watoto kunapswa kuwa kipaumbele. Ukiukwaji wa sheria utakuwa ni uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu."

Pillay amesema ukiukwaji wote wa sheria ya kimataifa ni lazima uchunguzwe vyema, kwa njia huru.