Jamii ya kimataifa yapaswa kusaidia Ethiopia kupokea wakimbizi wa Sudan Kusini- OCHA

23 Julai 2014

Tayari wakimbizi 180,000 wa Sudan Kusini wamepata hifadhi nchini Ethiopia baada ya kukimbia vita vinavyoendelea nchini mwao, asilimia 90 wakiwa ni wanawake na watoto wanaohitaji msaada wa dharura. Hayo yameripotiwa na John Ging, Mkuu wa Operesheni katika Ofisi ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu, OCHA, akizungumza na waandishi wa habari mjini New York baada ya ziara yake nchini Ethiopia.

Ging ameipongeza serikali ya Ethiopia kwa kujitolea kufungua mipaka yake na kukaribisha wakimbizi wa sudan Kusini, akionya pia kuwa idadi yao ikiendelea kuongezeka, itakuwa changamoto kubwa kwa wenyeji ambao tayari ni maskini, hapo akiuliza:

“ Swali sasa ni : jamii ya kimataifa inafanya nini? Nchi zingine zote 192 wanachama wa Umoja wa Mataifa wanafanya nini ? Je wanawajibika na kuisaidia Ethiopia kwa mzigo huo, na pia nchi nyingine zinazopokea wakimbizi? Na jibu hapa ni la, hawafanyi hivo. Inabidi tuone shida hiyo inatatuliwa duniani”

Amesema, mahitaji ya wakimbizi yamefadhiliwa kwa asilimia 25 tu, na kuna hatari ya kukumbwa na uhaba wa chakula ifikapo mwezi wa Septemba, akiongeza kwamba huduma za msingi kama vyoo na maji hazitolewi kwa kiwango kinachotakiwa. Amesema asilimia 30 ya watoto waliopo kambini wameugua utapiamlo, ambacho ni kiwango kilicho juu zaidi ya kiwango cha dharura.

Hatimaye, ametoa wito kwa viongozi wa Sudan Kusini, akisema wawili hao wamesababisha mzozo unaoharibu misingi mipya ya taifa lao changa, na wanapaswa kuachana na mgogoro wao wa kibinafsi ili kuokoa nchi ya Sudan Kusini na raia wake.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter