Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mahitaji ya kibinadamu yazidi kufurika Gaza

Hali ya uhai kutokana na vizingiti yanazidi kufifia Gaza na Ukanda wa Magharibi. Picha@ Shareef Sarhan/UNRWA

Mahitaji ya kibinadamu yazidi kufurika Gaza

Ofisi ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu na misaada ya dharura, OCHA, imesema kuwa inasikitishwa na ongezeko la mahitaji ya dharura ya kibinadamu Gaza kufuatia kuanza kwa operesheni za kijeshi za Israel mnamo Julai 7, ambazo zimeelezwa kuwa na lengo la kukomesha mashambulizi ya roketi kutoka Gaza.

OCHA imesema kuwa, mbali na mauaji na majeraha mengi dhidi ya raia, vituo 5 vya afya vimeharibiwa Gaza kutokana na mashambulizi ya angani ya Israel, ikiwemo hospitali moja ambako muuguzi alijeruhiwa wagonjwa walio mahtuti na watoto kulazimika kuondolewa.

Nalo Shirika la Afya Duniani, WHO, limesema kuwa machafuko Ukanda wa Gaza yamedhoofisha uwezo wa serikali na wizara ya afya katika maeneo ya Wapalestina yaliyokaliwa kuubeba mzigo ulioongezeka wa kutoa huduma za afya, na kutoa ombi la dharura la ufadhili ili kunusuru huduma za afya ambazo zimo hatarini kusambaratika.