Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNEA kuanza Nairobi, biashara haramu ya mazao ya porini kuangaziwa

Achim Steiner, Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP (Picha@UN-Radio)

UNEA kuanza Nairobi, biashara haramu ya mazao ya porini kuangaziwa

Mkutano wa kwanza wa Baraza la Mazingira la Umoja wa Mataifa, UNEA unaanza Jumatatu mjini Nairobi Kenya maudhui yakiwa ni malengo ya maendeleo endelevu na ajenda ya maendeleo baada ya mwaka 2015.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Nairobi, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa, UNEP, Achim Steiner ametaja moja ya mada zitakazoangaziwa ni uhalifu dhidi ya mazingira na usafirishaji haramu wa mazao ya porini.

Ametaja mazao hayo kuwa ni pamoja na mbao, vifaru na tembo akisema kuwa biashara ya haramu ya mazao hayo huleta karibu dola Bilioni 200 kila mwaka

(Sauti ya Steiner)

Mkuu huyo wa UNEP amesema washiriki wakiwemo mawaziri wa mazingira, wadau na mashirika ya kimataifa watajadili mbinu za kudhibiti biashara hiyo na uhalifu wa mazingira kwa kuweka ushirikiano zaidi baina ya mataifa zaidi ya ule wa sasa kupitia shirika la kimataifa la polisi.

Steiner amesema uhalifu wa mazingira unazidi kudumaza nchi, unazorotesha mifumo ya seriklia na hata kutishia uwepo wa wanyama na mimea porini.

Kuanzishwa kwa UNEA ni muitikio wa wanachama wa Umoja wa Mataifa walipokutana wakati wa Rio +20 nchini Brazili mwezi Juni mwaka 2012 na kutaka kuanzishwa kwa mamlaka simamizi ya shirika la mazinigira duniani, UNEP.

UNEA imechukua nafasi ya baraza simamizi la UNEP lililokuwepo tangu mwaka 1972 likiwa na wanachama 58 Kwa sasa UNEA inajumuisha nchi zote 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa na zile zenye hadhi ya uangalizi na wadau wengine ambapo wote wanashiriki kwenye mjadala.