Baraza Kuu laridhia uteuzi wa Sam Kutesa wa Uganda kuwa Rais wa mkutano wa 69 wa Baraza hilo.
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limeridhia uteuzi wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda, Sam Kutesa kuwa Rais wa mkutano wa 69 wa Baraza hilo.
Rais wa sasa wa baraza Kuu John Ashe alieleza kuwa Muungano wa Afrika ambao kwa sasa ndio una wajibu wa kushika wadhifa huo, uliwasilisha jina pekee la Kutesa na hivyo jina hilo limeridhiwa.
Akizungumza punde baada ya uteuzi Kutesa amesema ameshukuru kwa imani ambayo wamekuwa nayo kwake na mchango wa Uganda kwenye chombo hicho cha kimataifa.
Bwana Kutesa amesema kwa sasa kuna changamoto kubwa zinazokabili dunia lakini kwa pamoja nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa zinaweza kushirikiana na kukabiliana nazo.
Amesema umoja huo ndio umefanya chombo hicho kuendelea kuwa na umuhimu akitaja malengo ya maendeleo ya Milenia yanavyochochea mabadiliko.
Hata hivyo amesema ajenda ya maendeleo baada ya mwaka 2015 isipuueze misingi iliyowekwa na malengo ya milenia na iwe jumuishi kwa maeneo yote ya dunia.