Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tofauti za miji na vijijini ni changamoto kwa maendeleo: Dkt. Asha-Rose

Kuwezesha wakulima vijijini kutasaidia kuinua kipato cha wakazi wa maeneo hayo na kuondoa tofauti kati ya mijini na vijijini. (Picha@FAO-Tanzania)

Tofauti za miji na vijijini ni changamoto kwa maendeleo: Dkt. Asha-Rose

Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu nafasi ya haki za binadamu na utawala wa sheria kwenye ajenda ya maendeleo endelevu baada ya mwaka 2015 umeingia siku ya pili na mwisho hii leo ambapo aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja huo Dokta Asha-Rose Migiro amehutubia akisema kuwa suala hilo ni muhimu likapatiwa kipaumbele.

Dkt. Asha-Rose ambaye kwa sasa ni Waziri wa Sheria na Mambo ya Katiba waTanzania ametolea mfano wa nchi yake akisema imepiga hatua kwenye malengo ya milenia lakini bado kuna maeneo ya kufanyia kazi ikiwemo tofauti kati ya maeneo ya miji na vijini.

(Sauti ya dkt. Asha-Rose)

“Naamini kuna nchi nyingi zaidi zinakumbwa na tatizo hili! Tofauti za miji na mijini ni mojawapo ya maeneo lakini katika kutekeleza malengo ya milenia, maeneo mengine yalibainika! Ni jambo lisilo na mjadala kuwa haki za binadamu na utawala wa sheria ni mambo ya msingi kwa maendeleo.”