Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwaka 2014 uwe wa juhudi zaidi dhidi ya migogoro, umaskini na mabadiliko ya tabianchi: Ban

Mwaka 2014 uwe wa juhudi zaidi dhidi ya migogoro, umaskini na mabadiliko ya tabianchi: Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, amesema mwaka huu mpya unahitaji juhudi zaidi kidiplomasia, hatua zaidi dhidi ya umaskini na pia kuchukua hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.

Bwana Ban amesema hayo katika mkutano na waandishi wa habari mjini New York, ambako amezungumzia masuala muhimu yatakayoangaziwa mwaka. Bwana Ban amesema mwaka huu pia utakuwa muhimu kuhusu malengo ya maendeleo ya milenia, na hivyo basi hatua mathubuti zinatakiwa kufanywa kuhusu ajenda ya maendeleo baada ya mwaka 2015, fungu la malengo ya maendeleo endelevu na njia ya kifedha ya kuyatimiza malengo hayo.

Hata hivyo, Bwana Ban amesema migogoro na majanga ya mara kwa mara ni vikwazo vikubwa katika mikakati hiyo

“Tunapoangazia kujenga misingi hii ya kudumu ya maendeleo na amani, Umoja wa Mataifa pia unakabiliwa na wimbi la migogoro na majanga makubwa. Hivi vitahitaji uzingativu zaidi kutoka kwa jamii ya kimataifa- kisiasa, kirasilmali na uungwaji mkono. Hali Syria, Sudan Kusini na Jamhuri ya Afrika ya Kati imezidi kuzorota. Haya ni majanga yanayoweza kuepukika, ambayo yanawathiri mamilioni ya raia.”