Kampeni ya kuelekea miaka 20 baada ya azimio la utekelezaji la Beijing yazinduliwa rasmi leo: UN-Women
Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya wanawake, UN-Women leo limezindua rasmi kampeni ya mwaka mzima kuelekea miaka 20 tangu kufanyika kwa mkutano wa wanawake huko Beijing, China, lengo ni kufanya tathmini kuhusu uwezeshaji wanawake na jamii kwa ujumla. Taarifa zaidi na Priscilla Lecomte.
(Taarifa ya Priscilla)
Mpango wa utekelezaji wa azimio la Beijing wa mwaka 1995, ni ahadi kwa wanawake na wasichana ambayo haijatekelezwa ipasavyo, amesema hii leo Mkurugenzi Mtendaji wa UN-Women, Phumzile Mlambo-Ncguka katika uzinduzi wa kampeni hiyo iitwayo “Wezesha Wanawake ni Kuwezesha Ubinadamu: Wazia hilo!”.
Amesema licha ya mafanikio mathalani wasichana wengi kujiunga na shule na kumaliza, wanawake kwenye siasa bado kuna changamoto..
(Sauti ya Phumzile)
“Ukatili dhidi ya wanawake ni moja ya changamoto kubwa zaidi, umaskini ni changamoto kubwa pia, ukosefu wa usawa unaathiri wanawake zaidi kuliko wanaume, kwani ukiangalia kipimo cha wakosao usawa, wengi wao ni wanawake. Na umaskini pia wengi wao wenye njaa na maskini ni wanawake, na ukiangalia ukatili dhidi ya wanawake, wale wahanga na waathirika wengi ni wanawake kwa hiyo hizo ni baadhi ya changamoto za karne ya 21 ambazo tunapaswa kushughulikia.”
Hata hivyo amesema maadhimisho ya miaka 20 yamekuja wakati muafaka ambapo dunia inaandaa ajenda ya maendeleo baada ya mwaka 2015 ambapo hoja zitakazoibuka zitaweza kujumuishwa katika ajenda hiyo.
Kampeni hiyo ya kuelekea mwakani itahusisha matumizi ya mitandao ya kijamii, vyombo vya habari na mikutano ambapo mwezi huu mamia ya maelfu ya watu watakutana Sweden kufanya utetezi wa ulinzi wa haki za wanawake na wasichana, ilhali mwezi Novemba huko India, wanaume na wavulana watakuwa na kikao cha kushinikiza usawa wa kijinsia
Maadhimisho rasmi ya miaka 20 baada ya azimio la Beijing yatafanyika wakati wa kikao cha 59 cha Kamisheni kuhusu hadhi ya wanawake mwakani.