Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNFPA yasaka usaidizi kwa huduma za afya ya uzazi Sudan Kusini:

Mtoa huduma kutoka UNFPA akimsaidia mama aliyejifungua kwenye kambi ya wakimbizi wa ndani huko Juba. (Picha-UNFPA)

UNFPA yasaka usaidizi kwa huduma za afya ya uzazi Sudan Kusini:

Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na idadi ya watu UNFPA limesema kuwa mustakhabali wa wajawazito 200,000 huko Sudan Kusini mwaka huu pekee uko mashakani kutokana na mapigano yanayoendelea kuzidi kuporomosha miundombinu ya afya.

Mkurugenzi Mtendaji wa UNFPA Babatunde Osotimehin amesema hayo kwenye taarifa yake inayoenda sanjari na ripoti kutoka Wizara ya Afya Sudan Kusini kuhusu mlipuko wa ugonjwa wa Kipindupindu kwenye mji mkuu Juba.

Amesema wanawake 30,000 kati ya hao wanaweza kufariki dunia kutokana na kukosa huduma za msingi wakati wa kujifungua na hivyo amesema atatumia mkutano wa wahisani wa Sudan Kusini utakaofanyika Norway wiki ijayo kusihi usaidizi wa dola Milioni 25 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya afya ya uzazi Sudan Kusini na nchi jirani wanakombilia wakimbizi.

Dkt. Osotimehin amesema hata majanga yanapoibuka wanawake wanaendelea kubeba ujauzito na wanakabiliana na vikwazo vikubwa wanapohudumia wengine licha ya kuwa hatarini kukumbwa na utapiamlo, ukatili wa kingono, utumikishwaji na kubeba ujauzito usiopangwa.

Tangu mwezi Februari mwaka huu, UNFPA imepeleka Sudan Kusini wakunga 33 katika majimbo 10 nchini Sudan Kusini ambapo wajawazito 1,300 waliokabiliwa na matatizo wakati wa kujifungua walipatiwa huduma.