Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kiir na Machar kujadili mustakhbali wa nchi yao Addis Ababa: Ban

Katibu Mkuu wa UM Ban Ki-Moon akiagana na Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini mjini Juba. (Picha:UN /Eskinder Debebe)

Kiir na Machar kujadili mustakhbali wa nchi yao Addis Ababa: Ban

Katibu Mkuu wa Umoja  wa Mataifa Ban Ki-Moon amehitimisha ziara yake ya siku Moja huko Sudan Kusini ambapo baada ya mazungumzo na Rais Salva Kiir pia ameweza kuzungumza kwa njia ya simu na Riek Machar, Makamu wa zamani wa Rais anayeongeza upinzani.

Bwana Ban amewaambia waandishi wa habari kabla ya kuondoka Juba amezungumza na Machar kwa njia ya simu ambapo walisikilizana kwa taabu lakini kiongozi huyo wa upinzani amemtaarifu kuhusu mwaliko wa mazungumzo yatakayofanyika Addis Ababa Ethiopia tarehe Tisa mwezi huu.

Amemnukuu Machar akisema kuwa atajitahidi kuwepo Addis Ababa kushiriki mkutano huo kutokana na mwaliko wa Mwenyekiti wa IGAD Hailemariam Desalegn ambaye pia ni Waziri Mkuu wa Ethiopia.

Tayari Rais Kiir alishathibitisha kuwa atashiriki mkutano huo ili kupatia suluhu mzozo uliotumbukiza nyongo matarajio ya wananchi wa Sudan Kusini baada ya uhuru wa nchi yao miaka mitatu iliyopita.

Katika mkutano  huo Bwana Ban aliulizwa kuhusu tuhuma dhidi ya mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa Sudan Kusini, UNMISS Hilde Johnson na baadhi ya watendaji kuwa na uhusiano na kiongozi wa upinzani, ambapo amesema ripoti hizo ni uzushi usio na msingi wowote.

Amesema Rais Kiir ameahidi na kutangaza mbele ya umma kuwa na imani na uongozi wa UNMISS na kwamba anaunga mkono uongozi wa Bi. Johnson.