Jamii zenye amani na utulivu ni muhimu kwa maendeleo baada ya 2015: Ashe
Baraza kuu la Umoja wa Mataifa leo limeanza mjadala wa siku mbili kuhusu umuhimu wa jamii tulivu na zenye amani katika kufanikisha utekelezaji wa malengo endelevu baada ya mwaka 2015. Assumpta Massoi na ripoti kamili.
(Taarifa ya Assumpta)
Utulivu na amani ni muhimu katika kuwezesha maendeleo endelevu kama ilivyo ghasia ni moja ya vikwazo vikubwa vya maendeleo hayo, amesema Rais wa Baraza Kuu John Ashe katika hotuba yake ya ufunguzi.
Amesema ni jambo la kutia moyo kuwa vita na migogoro kati ya nchi na nchi vimepungua, lakini bado utulivu na ghasia ndani ya nchi vimeongezeka na kusababisha vifo na machungu kwa raia. Amesema hali hiyo ikiendelea suala la kutokomeza umaskini litabakia ndoto kwa wengi iwapo jamii ya kimataifa haitashirikiana kumaliza migogoro, ukosefu wa utulivu, kuongeza ujumuishi, uongozi bora na maendeleo kwa wote.
(Sauti ya Ashe)
“Kufikia lengo kuu la kutokomeza umaskini kutabakia ndoto kwa wengi iwapo hatutashirikiana kumaliza migogoro na ukosefu wa utulivu, halikadhalika kuongeza ujumuishi, uongozi bora, utawala wa kisheria, haki za binadamu na haki ya maendeleo kwa wote.”
Baraza lilihutubiwa pia na Katibu Mkuu Ban Ki-Moon ambaye naye amesema ni kweli mizozo ndani ya nchi imezidi na visababishi ni vingi ikiwemo mgao usio sawia wa rasilimali, kutengwa kisiasa, ufisadi na ukosefu wa njia bora za kuondoa machungu ya wananchi. Hivyo akasema..
(Sauti ya Ban)
Mizozo ya aina hii inaweza kusuluhishwa tu kwa njia kamilifu na shirikishi. Ndio maana mikakati yetu tuliyoandaa kwa Sahel na Maziwa Makuu Afrika unalenga maendeleo, amani na usalama, haki za binadamu na utawala wa kisheria.”