Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNMISS yakanusha madai ya kuhusika na kilichotokea Bentiu, Sudan Kusini

UNMISS yakanusha madai ya kuhusika na kilichotokea Bentiu, Sudan Kusini

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS umesema ripoti zilizotolewa na afisa mmoja mwanandamizi wa serikali nchini humo ya kwamba ujumbe huo unahusika kiasi na mauaji ya raia kwenye mji wa Bentiu jimbo la Unity hazina ukweli wowote.

Afisa huyo alidai kuwa raia waliokuwa wanajaribu kusaka hifadhi kwenye eneo la UNMISS walikataliwa kuingia na kwamba waliuawa baada ya kutakiwa kukimbilia kwenye kanisa, msikiti na hospitali mjini humo. Jose Contreras ni msemaji wa UNMISS.

(Sauti ya Contreras)

"Ujumbe wa Umoja wa Mataifa Sudan Kusini unakanusha jitihada zozote za kubebeshwa lawama za ukiukwaji wa haki za binadamu uliotokea mji wa Bentiu. Raia yeyote ambaye aliweza kufika eneo letu na ambao hawakuwa na silaha na walikuwa katika tishio dhahiri waliruhusiwa kuingia na pia tulipeleka walinda amani wetu huko Bentiu kuepusha raia na ghasia na hata kusafirisha idadi kubwa ya raia hadi kwenye eneo salama la hifadhi lililopo katika ofisi zetu.”

Halikadhalika Contreras amesema baadhi ya raia waliojaribu kuelekea eneo la UNMISS walizuiliwa kufanya hivyo na askari wa jeshi la Sudan Kusini ambao walikuwa wanalinda doria kwenye kituo kimoja cha ukaguzi.

Hadi sasa takribani raia Elfu Ishirini na Wawili wamesaka hifadhi kwenye ofisi za UNMISS huko Bentiu.