Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban alaani shambulio kwenye kambi ya UNMISS huko Bor

Ban alaani shambulio kwenye kambi ya UNMISS huko Bor

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon amelaani vikali shambulio la leo dhidi ya raia na walinda amani kwenye ofisi ya ujumbe wa kulinda amani wa Umoja huo Sudan kusini, UNMISS huko Bor, ambao ni mji mkuu wa jimbo la Jonglei.

Taarifa ya Msemaji wa Umoja wa Mataifa imemkariri Ban akisema kuwa kitendo cha kushambulia eneo linalohifadhi raia kinazidisha zaidi mvutano huku akikumbusha wahusika wa tukio hilo kuwa halikubaliki na ni uhalifu wa kivita.

Bwana Ban ametuma rambirambi kwa familia za wafiwa, akiwatakia ahueni ya haraka manusura wa shambulio hilo.

Katibu Mkuu ametoa wito kwa serikali ya Sudan Kusini kuchukua hatua za haraka kuhakikisha usalama kwenye maeneo yote ya UNMISS yanayohifadhi raia huku akitaka pande husika kujizuia kufanya vitendo vyovyote au kutoa maneno yanayoweza kuzorotesha zaidi usalama.