Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wananchi wa Guinea-Bissau wapiga kura Jumapili, Ban awatakia uchaguzi wa amani

Wananchi wa Guinea-Bissau wapiga kura Jumapili, Ban awatakia uchaguzi wa amani

Wananchi wa Guinea Bissau leo Jumapili wanapiga kura kuchagua rais na wabunge ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon ametoa wito kwa wananchi na taasisi nchini humo kuhakikisha uchaguzi huo unafanyika kwa amani na unakuwa huru na wa haki.

Bwana Ban amesema wagombea nafasi husika, wafuasi wao pamoja na serikali ya mpito na vyombo vinavyosimamia uchaguzi bila kusahau mashirika ya kiraia na wananchi wa ujumla wote wana dhima muhimu ya kufanikisha suala hilo.

Katibu Mkuu amekaririwa kwenye taarifa ya msemaji wake akieleza kuwa kuhitimishwa salama kwa mchakato wa uchaguzi kutawezesha kurejeshwa kwa utawala wa kikatiba Guinea-Bissau pamoja na usaidizi wa kimataifa uliokuwa umesitishwa.

Halikadhalika amesema kutawezesha kuwepo kwa utulivu wa kisiasa na utekelezaji wa mipango ya muda mrefu na kuendeleza amani na ujenzi wa taia hilo kiuchumi na kijamii kwa usaidizi wa wahisaji wa maendeleo.

Bwana Ban ametaka wagombea kuheshimu matokeo rasmi ya uchaguzi pindi yatakapotangazwa na Mahakama Kuu nchini humo na wafuate taratibu za kisheria kutatua masuala yoyote ya uchaguzi yanayoweza kuibuka.

Uchaguzi huu wa leo unakuwa wa kwanza tangu mwaka 2012 kulipofanyika mapinduzi ya kijeshi yaliyomwondoa madarakani Rais wa muda Raimundo Pereira.