Wadudu waenezao magonjwa bado ni tishio: Utashi wa kisiasa wahitajika: Ban

4 Aprili 2014

Wakati dunia inaelekea kwenye maadhimisho ya siku ya afya duniani tarehe Saba mwezi Aprili, Umoja wa Mataifa umesema magonjwa yanayoenezwa na wadudu kama vile mbu, kupe, konokono na inzi bado yameendelea kuwa tishio kwa binadamu.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon katika ujumbe wake wa siku hiyo amesema tishio la magonjwa hayo kwa binadamu liko dhahiri kwani kila mwaka zaidi ya watu Milioni Moja hufariki dunia kutokana na magonjwa yanayoenezwa na wadudu hao.

Magonjwa hayo ni pamoja na Malaria, kichocho, kidingapopo, homa ya manjano na matende ambayo ujumbe wa mwaka huu wa siku ya afya duniani umeyalenga kama njia ya kuimarisha jitihada za kuyatokomeza.

Bwana Ban amesema ni lazima nchi kujizatiti kukabiliana na wadudu hao huku akitanabaisha kuwa vita dhidi ya wadudu hao si ya sekta ya afya pekee bali inahusisha pia sekta nyingine kama vile ya mipango.

Mathalani amesema ukataji miti hovyo, ujenzi wa mabwawa au miradi ya umwagiliaji kwa ajili ya kuimarisha kilimo isipotekelezwa kiendelevu inaweza kuongeza mzigo wa magonjwa yanayoenezwa na wadudu.

Ametaka utashi wa kisiasa zaidi katika kufanya uamuzi wa masula hayo akisema kila mmoja ana dhima yake kutokomeza magonjwa hayo kuanzia taasisi za kimataifa, serikali, jamii na mtu mmoja mmoja.