Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yaanza kukusanya maoni ya umma kuhusu kiwango sahihi cha sukari

WHO yaanza kukusanya maoni ya umma kuhusu kiwango sahihi cha sukari

Shirika la afya duniani, WHO imezindua mpango wake wa kukusanya maoni ya umma juu ya rasimu ya mwongozo wa kiwango sahihi cha sukari kwa binadamu kwa siku.

Mwongozo huo ukikamilika utapatia nchi wanachama mwongozo wa jinsi ya kudhibiti matumizi ya sukari kama njia mojawapo ya kupunguza matatizo ya kiafya ikiwemo unene wa kupindukia na matatizo ya kuoza kwa meno.

Taarifa ya WHO inasema kuwa maoni juu ya rasimu hiyo yataanza kupokelewa kupitia tovuti ya shirika hilo www.who.int kuanzia tarehe Tano hadi 31 Machi mwaka huu na baada ya hapo jopo la wataalamu litapitia maoni hayo kabla ya rasimu hiyo kuhitimishwa.

Mwongozo wa sasa wa WHO kuhusu matumizi ya sukari unataka angalau mlo wa mtu kwa siku uwe na asilimia isiyozidi Kumi ya sukari lakini pendekezo jipya ni kupunguza kiwango hicho lakini kwa jumla kiwango cha mlo unaoongeza nguvu mwilini kipunguzwe hadi chini ya asilimia Tano ambacho ni sawa na vijiko sita vya sukari..

WHO inasema vyanzo vya sukari ni pamoja na ile mtu anayoongeza mwenyewe mathalani kwenye chai, lakini kiasi kingine kikubwa kinapatikana kwenye vyakula na vinywaji vinavyoandaliwa viwandani kama vile maji ya matunda na nyanya zilizosindikwa.

Mathalani WHO inasema soda ya kwenye kopo ina gramu 40 za sukari sawa na vijiko 10 vya chai vya sukari.