Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Viumbe wa porini ni sehemu ya urithi wetu na maendeleo endelevu: Ban

Viumbe wa porini ni sehemu ya urithi wetu na maendeleo endelevu: Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, amesema viumbe wa porini ni sehemu muhimu ya mustakhbali wa mwanadamu kwa sababu ya mchano wake katika sayansi, technolojia na starehe. Bwana Ban amesema hayo wakati akifungua maonyesho ya kuadhimisha Siku ya Viumbe wa Porini Duniani, ambayo inaadhimishwa leo kwa mara ya kwanza. Maonyesho hayo yameandaliwa na serikali zaThailand, Uingereza na Uswisi.

Ban amesema kuwa watu na tamaduni nyingi zimetegemea bayoanuai ya mimea na wanyama wa pori kwa chakula, mavazi, dawa na hata kuendeleza maisha yao kiroho, na hiyo viumbe hao ni sehemu ya urithi wa wanadamu na maendeleo endelevu.

Hata hivyo, licha ya thamani hiyo, Bwana Ban amesema viumbe wa porini wamo hatarini kwa sababu ya ukataji miti, mabadiliko ya tabianchi, mienendo ya matumizi ya ardhi, matumizi mabaya ya ardhi na bahari, pamoja na uwindaji haramu wa mimea na wanyama wa porini.

Amesema ni muhimu kuongeza uelewa siyo tu wa thamani ya viumbe wa porini, lakini pia hali inayosikitisha ya kupungua kwa viumbe hao katika dunia ya sasa.