Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban apongeza EU kwa hatua ya awali ya kuhusu mabadiliko ya tabianchi

Ban apongeza EU kwa hatua ya awali ya kuhusu mabadiliko ya tabianchi

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon ambaye yuko Uswisi kwa ziara ya kikazi hii leo amezungumza na waandishi wa habari huko Davos na kusema anatiwa sana moyo kuona suala la mabadiliko ya tabianchi yanapatiwa kipaumbele.

Bwana Ban ametolea mfano Kamisheni ya Ulaya ambayo amesema imetangaza pendekezo la matamanio makubwa ya kupunguza viwango vya gesi chafuzi kwa asilimia 40 ifikapo mwaka 2040 na kuweka lengo la kuwa na nishati mbadala kwa asilimia 27 katika kipindi hicho hicho.

Amesema mfano huo ni wa kuigwa wakati huu dunia iko kwenye mchakato wa kukamilisha makubaliano mapya kuhusu mabadiliko ya tabianchi hapo mwakani.

Bwana Ban amekumbusha kuwa mwezi Septemba mwaka huu ataandaa mkutano wa mabadiliko ya tabianchi mjini New York ambapo alipoulizwa na waandishi matarajio yake, Bwana Ban amesema ni makubwa kwani utakuwa mkutano wa vitendo na si maneno matupu.

Amesema ni matumaini yake kuwa wakati wa mkutano huo, viongozi wa Umoja wa Ulaya watakuwa wameridhia mapendekezo yao na hivvyo kuwa mfano kwa mataifa mengine.