Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wananchi Sudan Kusini wamekata tamaa wanataka wahamishwe: Mkuu OCHA

Wananchi Sudan Kusini wamekata tamaa wanataka wahamishwe: Mkuu OCHA

Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa masuala ya usaidizi wa kibinadamu Bi. Valerie Amos ametembelea Malakal ambao ni mji mkuu wa jimbo laUpper Nilenchini Sudan Kusini na kushuhudia hali ya taabani inayokumba maelfu ya raia walio kwenye makazi ya muda ndani ya ofisi ya ujumbe wa Umoja huo, UNMISS.

Bi. Amos ambaye pia ni mkuu wa ofisi ya uratibu wa masuala ya kibinadamu OCHA, ameshtushwa na kile alichokiona ikiwemo makazi kuharibiwa, maelfu ya watu kusaka hifadhi kwenye hospitali ya mafunzo ya tiba huko Malakal huku huduma zikizorota kila uchao.

(Sauti ya Valerie)

Watu wana hofu kubwa, hawataki kutoka nje, wanatueleza kuwa wanataka kuhamishiwa nchi nyingine. Kuna hitaji la haraka la maridhiano, watu kuhakikishiwa ulinzi na usalama wao, kuna hatari ya mlipuko wa magonjwa kwenye kambi hizi za muda zilizoibuka na zimejaa watu wengi bila huduma ya kutosha ya maji na chakula.”

Bi. Amos amesema mazungumzo yake na wananchi hao yamedhihirisha kuwa wamepoteza imani na wanataka kuondoka kabisa na kuelekea maeneo mengine ya Sudan Kusini au nje ya nchi hiyo kabisa. Amesisitiza umuhimu wa maridhiano kwani wananchi hao wamepitia machungu mengi.