Ban akutana na Waziri wa Iran wa masuala ya nchi za Kiarabu na Afrika

14 Januari 2014

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, leo amekutana na kufanya mazungumzo na Hossein Amir Abdollahian, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislam ya Iran anayehusika na masuala ya nchi za Kiarabu na Afrika.

Katika mkutano huo ambao ulifanyika pembezoni mwa kongamano la pili la kutoa ahadi za ufadhili kwa ajili ya Syria, wawili hao walijadili mzozo wa Syria na kuzungumzia kujitoa kwao kusaidia katika hali ya kibinadamu na kuwafikishia waathirika misaada.

Wamejadili pia mtazamo wa Iran kuhusu mikakati ya kikanda ya kisiasa ambayo inaweza kwenda sambamba na mkutano wa kimataifa kuhusu Syria na mazungumzo baina ya serikali na makundi ya upinzani. Wamesema wote wanaamini kuwa hakuna suluhu la kijeshi kwa mzozo huo, ila suluhu la kisiasa kupitia mazungumzo. Ban pia amekaribisha kuanza kutekelezwa makubaliano kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran mnamo Januari 20.