Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban azungumzia masuala muhimu kuelekea kuanza kikao cha 68 cha Baraza Kuu

Ban azungumzia masuala muhimu kuelekea kuanza kikao cha 68 cha Baraza Kuu

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon amesema wakati kikao cha 68 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kinaanza leo, ni wakati muafaka wa ushirikiano duniani hususan kwa kuzingatia changamoto ya amani, ulinzi, usalama na usaidizi wa kibinadamu nchini Syria. Ikiwa ni utaratibu wake wa kawaida kuzungumza na waandishi wa habari kabla ya kuanza rasmi kwa kikao kipya cha Baraza Kuu, Bwana Ban amesema lazima ifahamike kuwa matumizi ya silaha za kemikaliSyriani sehemu ndogo tu ya madhila wanayokumbana nayo wananchi wa Syria. Hivyo amesema atatumia kusanyiko la wiki ijayo la viongozi mbali mbali duniani kuwaeleza kuwa machungu yaSyriani lazima yaishe na hatua sasa zichukuliwe.  Katibu Mkuu amesema suala lingine muhimu ni ajenda ya maendeleo baada ya mwaka 2015, hivyo..

 “Mjadala wa dunia kuhusu ajenda  baada ya mwaka 2015 nao unaendelea. Nitatumia tukio muhimu la siku ya Jumatano kuzindua rasmi ripoti yangu iitwayo Maisha ya hadhi kwa wote.. ambayo inajumuisha dira yangu kuhusu mabadiliko tunayohitaji. Mwezi huu pia tutashuhudia uzinduzi wa ripoti muhimu: tathmini mpya zaidi kuhusu mabadiliko ya tabianchi. Ujumbe wake hautamshangaza mtu: joto liko kwetu sote.”

Halikadhalika amesema atatumia wiki ijayo atakapokutana na viongozi kutoka sehemu mbali mbali duniani kuwaeleza umuhimu wa kuwekeza kwa wananchi wao, kuwasikiliza na hata kuweka mustakhbali sahihi kwa maendeleo endelevu ya wananchi wote.