Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mshikamano ni suluhu ya kutatua migogoro inayokumba dunia: Ban

Mshikamano ni suluhu ya kutatua migogoro inayokumba dunia: Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon ametoa ujumbe wake wa siku ya kimataifa ya mshikamano kibinadamu hii leo na kusema mshikamano ndio njia pekee ya kutatua migogoro inayokumba dunia ya sasa yenye mwingiliano mkubwa. Ujumbe wa mwaka huu ni ubia wa kimataifa kwa ustawi wa pamoja.

Amesema siku hii ni muhimu zaidi kwa kuwa inasherehekewa wakati wa kipindi cha mpito ambapo watu duniani kote wanataka uhuru zaidi wa kisiasa, uwajibikaji na usawa na hivyo kutokana na mwingiliano wa mataifa kiuchumi, kijamii na hata mazingira, mshikamano ndio suluhisho pekee.

Halikadhalika Bwana Ban amesema mwaka huu dunia imeshuhudia tukio la kipekee la mshikamano kwenye mkutano wa Rio+20 ambapo serikali, taasisi za kiraia za kimataifa na sekta binafsi walikubaliana kujenga dunia ya baadaye ambayo ni endelevu kiuchumi, kijamii na kimazingira.

Amesema makubaliano hayo yatafikiwa iwapo kuna mshikamano na  hivyo ametaka siku hii iwe fursa ya kila mkazi wa dunia kuendeleza ajenda ya mshikamano ili kufikia malengo ya pamoja ikiwemo yale ya maendeleo ya milenia na ajenda ya maendeleo baada ya mwaka 2015.