Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yaitisha kikao cha dharura kuhusu kirusi Zika

WHO yaitisha kikao cha dharura kuhusu kirusi Zika

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani, WHO Dkt. Margaret Chan ameamua kuitisha mkutano wa kamati ya kimataifa ya kanuni za afya ili kujadili iwapo mlipuko wa virusi vya Zika unasababisha dharura ya kimataifa ya afya.

Akizungumza kwenye kikao cha bodi tendaji ya shirika hilo leo mjini Geneva, Uswisi, amesema kikao hicho kitafanyika tarehe Mosi mwezi ujao wakati huu ambapo kirusi hicho kimeripotiwa katika nchi 23 hata kwenye maeneo ambayo wakazi wake hawana kinga dhidi yake na kwamba…

(Sauti ya Dkt. Chan)

“Uwezekano wa uhusiano wa kirusi hicho na watoto wanaozaliwa na vichwa vidogo, kutokuwepo kwa chanjo, tiba mahsusi na vipimo vya kubaini haraka. Halikadhalika, mazingira yanayohusiana na mwelekeo wa El Nino mwaka huu yanatarajiwa kuongeza idadi ya mbu kwenye maeneo mengi. Kiwango cha wasiwasi ni kikubwa sambamba na sintofahamu. Maswali ni mengi, tunahitaji kupata majibu haraka.”

WHO katika tovuti yake imeweka maelezo ya kina kuhusu kirusi cha Zika, kinavyoenea na jinsi ya kujikinga.