Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jamii ya kimataifa ongeza usaidizi CAR na Cameroon: OCHA

Jamii ya kimataifa ongeza usaidizi CAR na Cameroon: OCHA

Naibu Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu uratibu wa misaada ya kibinadamu Kyung-Wha Kang amehitimisha ziara yake ya siku saba huko Cameroon na Jamhuri ya Afrika ya Kati akitoa wito kwa jamii ya kimataifa kusaidia harakati za kibinadamu kwenye nchi mbili hizo.

Wito wake unatokana na hali aliyoshuhudia mathalani Cameroon ambako kuna wimbi la wakimbizi kutoka CAR halikadhalika ongezeko la watu kukimbia makazi yao kaskazini mwa nchi hiyo kutokana na mashambulizi ya Boko Haram.

Akizungumza mwishoni mwa ziara yake bhi. Kyung-Wha ambaye pia ni naibu mkuu wa OCHA amesema zaidi ya watu Milioni Mbili nchini Cameroon wanahitaji misaada ya kibinadamu.

Halikadhalika mashariki mwa nchi hiyo, wakimbizi zaidi ya 150,000 kutoka CAR wamesaka hifadhi tangu kuzuka kwa mapigano nchini mwao.

Amesema hali zao za maisha ni za taabu akieleza wasiwasi wake kuhusu ongezeko la athari za mashambulizi yanayofanywa na Boko haram dhidi ya nchi jirani na Nigeria ikiwemo utekaji nyara raia na utumikishaji watoto kwenye mapigano.