Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Usalama kwa walinda amani ni muhimu: Kutesa

Usalama kwa walinda amani ni muhimu: Kutesa

Wakati kamati maalum ya Umoja wa Mataifa kuhusu operesheni za ulinzi wa amani ikitimiza miaka 50 mwaka huu tangu kuanzishwa kwake, Rais wa Baraza Sam Kutesa amesema shughuli za ulinzi wa amani zinaendelea kukumbwa na changamoto kila uchao licha ya mafanikio yaliyopatikana.

Akizungumza kwenye ufunguzi wa kikao cha kamati hiyo, Kutesa ametaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na usalama kwa walinda amani na raia akitaka hatua za dhati zichukuliwe kulinda makundi hayo dhidi  ya vitisho vinavyoibuka dhidi yao.

Bwana Kutesa amekaribisha tathmini inayofanywa na jopo la ngazi ya juu kuhusu operesheni hizo aksiema ni muhimu zikawa thabiti ili zisaidie siyo tu kulinda amani na usalama bali pia ziwezeshe upokonyaji silaha makundi yaliyojihami, michakato ya kisiasa na haki za binadamu.

Hata hivyo amesema..

(sauti ya Kutesa)

“Hii itahitaji usaidizi endelevu kutoka  Umoja wa Mataifa na ushirikiano wa kina kutoka nchi husika pamoja na zile zinatoa askari na polisi bila kusahau taasisi za kikanda katika utungaji wa sera na kuchukua uamuzi.”

Amesema ni kwa mantiki hiyo mwezi Mei mwaka huu anaitisha mkutano wa ngazi ya juu kuhusu uimarishaji uhusiano kati ya Umoja wa Mataifa na taasisi za kikanda.