Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chuja:

Habari Mpya

FAO kutabiri ongezeko la mavuno ya mpunga mwaka huu

Shirika la UM juu ya Chakula na Kilimo (FAO) limetabiri kwenye ripoti iliotolewa Ijumanne, kwamba mavuno ya mpunga mwaka huu yataongezeka kwa jumla ya asilimia 1.8, kiwango ambacho ni sawa na tani milioni 12 ziada za mpunga. Muongezeko huu utashuhudiwa zaidi katika nchi za Asia zinazopandisha nafaka hizo – mathalan, Bangladesh, Uchina, Bara Hindi, Indonesia, Myanmar na pia Phillippines na Thailand. Kadhalika uzalishaji wa mpunga unatarajiwa kuongezeka katika Afrika, Amerika ya Kusini na mataifa wanachama wa Umoja wa Ulaya, lakini katika Ujapani mavuno ya mpunga yatateremka, ikiwa moja ya mataifa machache ambayo bei za uzalishaji wa mpunga ziliporomoka mwaka jana.

UM waadhimisha Siku ya Kuhadharisha juu ya Ugonjwa wa Akili wa Watoto (Autism)

Ijumatano, tarehe 02 Machi 2008 iliadhimishwa na UM, kwa mara ya kwanza kihistoria, ni Siku ya Kuongeza Hisia za Kimataifa kuhusu Ugonjwa wa Akili wa Watoto (Autism). Risala ya KM ya kuihishimu siku hii ilipongeza ujasiri wa watoto waliodhuiwa na maradhi haya ya akili, na pia wazee wao ambao kila siku "hukabiliana na ulemavu wa vizazi vyao kwa mchanganyiko wa nia thabiti, kipaji cha kubuni na matarajio ya kutia moyo." Baraza Kuu la UM lilipitisha mwaka jana mnamo mwezi Disemba 2007 azimio la kuifanya tarehe 2, kila mwaka, kuwa ni Siku ya Kuongeza Hisia za Kimataifa kuhusu Ugonjwa wa Akili wa Watoto (Autism). Maradhi haya humnyima mtoto anayepatwa nayo uwezo wa kuwasiliana na wenziwake, na hushindwa kuendeleza uhusiano wa kijamii, na mara nyingi watoto huonesha tabia isiyo ya kikawaida na inayofurutu ada.

BU limeongeza muda wa vikwazo dhidi ya majeshi ya mgambo katika JKK

Ijumatatu, asubuhi, kwa saa za New York, Baraza la Usalama limepitisha, kwa kauli moja, azimio nambari 1807 (2008) ambapo wajumbe wa Baraza walipendekeza muda wa mamlaka ya ile Tume ya Wataalamu wanaofuatilia utekelezaji wa vikwazo vya silaha dhidi ya makundi ya wanamgambo katika JKK uendelezwe hadi Disemba 31 (2008).

Ukuaji wa uchumi na amani Usomali hutegemea zaidi michango ya wahisani wa kimataifa

Mkutano wa hadhi ya juu wa siku mbili, ulioandaliwa na Benki Kuu ya Dunia pamoja na UM kuzingatia \'Masuala ya Fedha na Uchumi Maendeleo kwa Usomali\', uliofanyika mjini Nairobi, Kenya wiki iliopita, ulihitimisha mijadala yake Ijumamosi ya Machi 29 ambapo kulitolewa mwito maalumu ulioitaka jamii ya kimataifa, pamoja na Usomali wenyewe, kukithirisha shirika huduma za kuleta maendeleo, mchango ambao ukitekelezwa natija zake zitaharakisha utulivu na amani katika nchi.

Waburundi 300,000 wamesaidiwa kurejea mwakao na UNHCR

Operesheni za Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) za kuwarejesha makwao, kwa khiyari, wahamiaji wa Burundi waliokuwa wakiishi kwenye kambi za muda ziliopo taifa jirani la Tanzania, kadhia zilizoanzishwa mwaka 2002, zilikamilisha kurejesha jumla ya wahamiaji 300,000 mnamo mwezi Machi mwaka huu.

Dhamira ya vidio ya 'Fitna' yalaaniwa na jamii ya kimataifa

Mataifa wanachama pamoja na KM wa Umoja wa Nchi za Kiislam yakijumuika vile vile Mataifa ya Ulaya wamelaani kipamoja vikali ile vidio iliotengenezwa na Geert Wilders, mwanabunge wa Uholanzi ambayo walisisitiza ilijaa \'kufuru\' dhidi ya WaIslam, na pia ilionesha chuki kwa wageni, na wanakhofia huenda ikasababisha utovu wa ustahamilivu wa kidini ulimwenguni. Kadhalika wanaamini dhamira hasa ya vidio hiyo, iliopewa jina la \'Fitna\' na iliosambazwa kwenye mtandao tangu wiki iliopita ilikuwa ni kuchochea chuki na vurugu miongoni mwa wafuasi wa dini.

BK lazingatia hatua za kuyafikia Malengo ya Milenia (MDGs) kwa wakati

Ijumatatu Baraza Kuu la UM limeanzisha kikao maalumu, hapa Makao Makuu, cha siku mbili, cha wawakilishi wote kujadilia taratibu za kuzijumuisha serikali za kimataifa pamoja na wadau wanaohusika na huduma za maendeleo, ili kuharakisha mchango wao wa kuyafikia yale Malengo ya Milenia (MDGs), kwa wakati, katika nchi masikini, kabla ya 2015 kumalizika.