Ukuaji wa uchumi na amani Usomali hutegemea zaidi michango ya wahisani wa kimataifa
Mkutano wa hadhi ya juu wa siku mbili, ulioandaliwa na Benki Kuu ya Dunia pamoja na UM kuzingatia \'Masuala ya Fedha na Uchumi Maendeleo kwa Usomali\', uliofanyika mjini Nairobi, Kenya wiki iliopita, ulihitimisha mijadala yake Ijumamosi ya Machi 29 ambapo kulitolewa mwito maalumu ulioitaka jamii ya kimataifa, pamoja na Usomali wenyewe, kukithirisha shirika huduma za kuleta maendeleo, mchango ambao ukitekelezwa natija zake zitaharakisha utulivu na amani katika nchi.
Wakati huo huo, Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) imeripoti kwamba hali ya wahka na mashaka bado inaendelea kutanda kwenye sehemu nyingi za Kati ya Kusini ya Usomali, ambapo iliripotiwa mapambano makali yalizuka wiki iliopita, baina ya yale makundi yanayopinga serikali, dhidi ya vikosi vya Serikali ya Mpito, vilivyokuwa vikisaidiwa na majeshi ya Ethiopia.